Maadhimisho ya 17 Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo

Maadhimisho ya 17 Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo

Posted 5 years ago

Oktoba 10, 2019

 

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinaungana na Jumuiya ya Kimataifa na wapenda haki kote ulimwenguni katika maadhimisho ya 17 ya kupinga adhabu ya kifo. Siku hii huadhimishwa tarehe 10 ya mwezi Oktoba kila mwaka ikiwa na lengo la kuhamasisha kufutwa kwa adhabu ya kifo katika nchi zinazokumbatia adhabu hiyo.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu ni mwanachama wa mtandao wa kupinga adhabu ya kifo duniani ‘’World Coalition Against Death Penalty’’ na tunaendelea kuelimisha umma juu ya madhara yanayoweza kutokana na adhabu hiyo sambamba na kuhamasisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kubadilisha adhabu hiyo kuwa adhabu ya kifungo cha Maisha. Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania,  2018 jumla ya watu 480 wapo kwenye orodha ya watu waliohukumiwa adhabu ya kifo wakiwa gerezani kusubiri kunyongwa.

Ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 inalinda haki ya kuishi kwa kila mtu. Hata hivyo, ibara hii inaathiriwa na Sura ya 16 ya Sheria za Makosa ya Jinai zinazoweka adhabu ya kifo kwa kosa la uhaini, mauaji na ugaidi.

Pamoja na mtazamo chanya ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo kauli aliyoitoa  mwaka 2017  akiwa anamuapisha Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahim Hamisi Juma akieleza nia yake ya dhati ya kutokutia saini adhabu hiyo kwa ajili ya utekelezaji pamoja na kuwasamehe wafungwa 61 waliohukuwiwa kunyongwa katika sherehe za uhuru mwaka 2017; bado Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinasisitiza uwepo wa utayari wa kufutwa kwa adhabu hiyo katika sheria zetu na kuwa na adhabu ya kifungo cha maisha kama adhabu mbadala.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu tunapinga adhabu hii ya kikatili na inayotweza utu kwa sababu kuu zifuatazo:

  1. Adhabu ya kifo ni adhabu ya kikatili na inakiuka haki ya msingi ya kuishi na kudumisha utamaduni wa ‘jicho kwa jicho’; Adhabu hii inapingana na misingi ya haki za binadamu kwa vile ni adhabu ya kikatili inayokatisha haki ya binadamu ya kuishi;
  2. Adhabu hii ikishatekelezwa haiwezi kubadilishwa, hata kama kuna makosa yametokea. Ni kama vile maji yakimwagika, hayawezi kuzoleka. Na tukumbuke kwamba mfumo wetu wa haki jinai bado una changamoto nyingi. Adhabu hii ikitolewa kwa mtu asiye na hatia kimakosa huwezi kuirekebisha. Kuna mifano mingi katika nchi mbalimbali ulimwenguni ambapo watu walinyogwa hadi kufa kwa maamuzi ya mahakama na baadae kuthibitika kwamba hawakutenda makosa yaliyopelekea adhabu ya kifo;
  3. Nchi nyingi duniani zimeendelea kuondoa adhabu ya kifo na kuacha kutekeleza adhabu hiyo. Kwa  mujibu wa ripoti ya shirika la kimataifa la Amnesty International ya mwaka 2018, jumla ya nchi 106 duniani zilikuwa zimeondoa adhabu ya kifo kwenye sheria zao kufikia mwezi Disemba 2017. Pia, jumla ya nchi 142 aidha zilikuwa zimeondoa adhabu hiyo au kuacha kuitekeleza. Kwa upande wa Afrika, takribani nchi 20 za kusini mwa Jangwa la Sahara zimeondoa adhabu hiyo, ikiwemo Guinea Bissau, Djibouti, Afrika Kusini, Senegal, Rwanda, Burundi, Togo, Gabon na Congo-Brazzaville. Kwa mwaka 2017, asilimia 84% ya adhabu za kifo zilizotekelezwa zilitekelezwa katika nchi 4 duniani;
  4. Mnamo Oktoba 2, mwaka huu 2019, nchi ya Angola imeridhia mkataba wa nyongeza wa hiari kwenye mkataba wa kimataifa wa haki za kisiasa na kiraia wa 1966 na kufuta adhabu ya kifo katika nchi zao na hivyo kufanya idadi ya nchi zilizoridhia mkataba huo kufikia 88;
  5. Waathirika wengi wa adhabu hii ni watu maskini ambao hawana uwezo wa kupata mawakili wabobevu kuwawakilisha katika kesi zao;
  6. Ni vigumu kuhakikisha kuwa inatekelezwa tu kwa wale watu ambao wametenda na kukutwa na hatia ya kosa hili au wabaya zaidi;
  7. Adhabu hii haimpi nafasi mtuhumiwa kujirekebisha bali ni ya kulipiza kisasi. Haimsaidii mtu yeyote hata familia ya muathirika;
  8. Hakuna ushahidi wowote kuwa adhabu hii inasaidia kuzuia au kupunguza makosa yanayopelekea adhabu hiyo kutolewa. Kwa mfano, nchini Marekani, ambapo adhabu hiyo inatekelezewa kwa kiasi kikubwa, bado matukio ya mauaji yamekuwa yakiongezeka na sio kupungua. Kwa upande mwingine, nchini Canada, ambapo adhabu hiyo iliondolewa mwaka 1976, matukio ya mauaji yamekuwa yakiendelea kupungua, huku mwaka 2016 yakiripotiwa matukio machache zaidi tangu mwaka 1966.
  9. Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwa taifa lililo katika mwelekeo wa kufuta adhabu ya kifo kwani mara ya mwisho adhabu hiyo kutekelezwa ni mwaka 1994, takribani miaka 25 iliyopita. 

Katika maadhimisho ya mwaka huu 2019, dhima kuu inaangazia namna ambavyo adhabu ya kifo huacha madhara kwa watoto na familia ambao wazazi/walezi wao wamehukumiwa adhabu ya kifo. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeandaa Makala fupi ya video ikionesha simulizi ya wazee watatu kati ya watano ambao walihukumiwa kunyongwa kwa kosa la pamoja la mauaji, baadaye wakapunguziwa adhabu na kuwa adhabu ya kifungo cha Maisha na hatimaye wakaachiwa huru kwa msamaha wa Rais John Pombe Mgufuli. Kisa hiki kinaonesha namna ambavyo udhaifu wa mifumo ya utoaji haki unavyoweza kupelekea uonevu na jinsi ambavyo utekelezaji wa adhabu ya kifo unavyoweza kuwanyima washtakiwa nafasi ya kujitetea. Makala hii pia inaonesha namna ambavyo familia, hususani watoto, wanavyoathiriwa na kitendo cha wazazi au walezi kuhukumiwa adhabu ya kifo.

Kufuatia sababu hizi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kinatoa wito kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuta adhabu hii katika sheria zinazoainisha kosa hilo na kuweka mbadala wa adhabu hiyo ikiwemo kifungo cha maisha au adhabu nyingine isiyohusisha kuua. Lengo la wito huu si kuwatetea wahalifu bali ni kupunguza madhara ya adhabu hii ya kikatili kwa jamii na kuendelea kulinda haki ya kuishi.

 

Imetolewa na;

Bi. Naemy Sillayo (Wakili)

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji