LHRC yazindua Ofisi Mpya jijini Dodoma

LHRC yazindua Ofisi Mpya jijini Dodoma

Posted 5 years ago

Septemba 26, 2019, Dodoma-Tanzania

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimezindua ofisi yake katika Makao Makuu ya nchi jijini Dodoma. Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimezundua ofisi hiyo kama sehemu ya kudumisha mahusiano ya kikazi na taasisi za serikali, Bunge pamoja na mahakama hasa kwa kuzingatia kuwa ukiacha Bunge, taasisi zote za serikali zimehamia jijini Dodoma kufuatia dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Dodoma kuwa Makao Makuu ya nchi.

Katika hafla hiyo ya uzinduzi mgeni rasmi alikuwa ni Mhe. Kangi Lugola, Waziri wa Mambo ya Ndani, wadau kutoka sekta mbalimbali ikiwemo Serikali, Bunge, Mahakama, taasisi za dini, asasi za kiraia, vyombo vya habari na wadau wa maendeleo wameshiriki. Kupitia hafla hiyo, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu pia kimezindua rasmi kampeni ya kusheherekea miaka 25 ya kuanzishwa kwa LHRC sambamba na Tuzo za Majimaji – tuzo zenye lengo la kutambua mchango wa watu wanaopigania haki za binadamu na utawala wa sheria nchini Tanzania.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi ya LHRC Dodoma iliyoko Area D, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Anna Henga amesisitiza kwamba lengo la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kufungua ofisi Dodoma ni kuimarisha mahusiano ya kikazi baina ya LHRC na Serikali kwa lengo la kudumisha ulinzi wa haki za binadamu na utawala bora nchini.

“Kuanzishwa kwa ofisi hii jijini Dodoma imetokana na msukumo usiozuilika wala kukwepeka wa kudumisha mashirikano na serikali na wadau wengine katika kupeperusha bendera ya haki za binadamu, uwajibikaji na utawala bora. Na sisi kama wadau wakubwa kwa serikali tumeona ni vyema kuunga mkono jitihada za serikali za kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi kwa vitendo. Na tunajivunia kwamba wakati tukiadhimisha miaka 24 ya utetezi wa haki za binadamu tumeweza kutanua wigo wetu kuwafikia wananchi wengi zaidi kwani kwa sasa wananchi wa mikoa ya kanda ya kati na maeneo ya karibu wanaweza kutufikia moja kwa moja”. Amesema Anna Henga.

Anna Henga amemshukuru Mhe. Kangi Lugola kwa kukubali ombi la Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo na kumsihi kudumisha mashirikiano hayo yenye tija katika kuwasaidia Watanzania wenye changamoto za kisheria na wanaovunjiwa haki zao bila msaada.

“.. nakushukuru sana kwa kukubali kutenga muda wako na kujumuika nasi katika tukio hili la kihistoria … tumeendelea kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali, Bunge na Mahakama. Kituo tunafanya kazi kwa karibu sana na Wizara Mbalimbali ikiwemo wizara unayoisimamia - Wizara ya Mambo ya Ndani na mamlaka mbalimbali za serikali. Hii yote ni katika kuhakikisha ujenzi wa nchi yetu pendwa unakuwa jumuishi na wenye manufaa kwa kila mwanajamii”. Aliongeza Anna Henga.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Anna Henga aliwashukuru wadau mbalimbali kwa kuendelea kuiunga mkono LHRC na zaidi aliwatambua kipekee waanzilishi wa LHRC pamoja na Wakurugenzi waliopita kwa mchango wao wa kuhakikisha uendelevu wa LHRC.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika hafla hiyo, Mhe. Kangi Lugola amewapongeza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kazi kubwa ya utetezi wa haki za binadamu wanayoifanya nchini huku akisisitiza kuwa kazi ya LHRC ni muhimu katika taifa lolote linalofuata misingi ya demokrasia na utawala wa sheria. Mhe. Lugola pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji (Mstaafu) wa LHRC na amewataka LHRC kuendelea kuenzi mchango wake.

“Napenda kuwapongeza Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kwa kutimiza miaka 24 na zaidi kwa kuzidi kukua kama mtetezi wa kweli wa haki za binadamu. Miaka 24 ni mingi na ni sehemu ya historia nzuri katika taifa letu linalofuata misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria. Kwa kipindi chote hicho mmefanya kazi ya kujitolea ya kuwafikia watanzania na kuwawezesha katika mambo mbalimbali hususani kuwajengea uwezo kwenye nyanja za sheria, utawala bora, elimu ya uraia na haki za binadamu kwa upana wake. Nawapongezeni na nazidi kuwatakieni kheri katika kufanisha malengo yenu mliojiwekea”. Amesema Mhe. Lugola

Mhe. Kangi Lugola pia amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuunga mkono kazi kubwa inafofanywa na LHRC na itadumisha ushirikiano kwa lengo la kujenga jamii inayoheshimu haki za binadamu na utawala wa sheria.

“..sisi kama serikali tutaendelea kuwaunga mkono na kushirikiana nanyi katika masuala mbalimbali yenye maslahi mapana kwa nvhi yetu. Wizara ya Mambo ya Ndani tumetoa na tutaendelea kutoa ushirikiano mzuri na wenye manufaa kwa jamii ya watanzania ili kufanikisha lengo kuu la serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. Rais. Dkk. Joseph Pombe Magufuli”. Ameongeza Mhe. Lugola

Ofisi hii ya Dodoma mbali na kutumika kama kiungo baina ya LHRC na Serikali, pia itatumika kuwafikia wananchi wa Kanda ya Kati na maeneo ya karibu kwa elimu kwa umma na msaada wa kisheria. Ofisi ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu jijini Dodoma ni ofisi ya nne baada ya ofisi kuu (ofisi ys Makao Makuu) iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam, ofisi ya Kituo cha Msaada wa Kisheria iliyopo mtaa wa Isere, Kinondoni – Dar es Salaam pamoja na ofisi ya Arusha iliyopo Sakina Kwa Idd.

 

Anuani ya ofisi ya Dodoma ni:

Kitalu na 22. Area D,

S.L.P 2289, Dodoma, Tanzania

Simu/Nukushi: +255 262350050

Barua pepe: lhrc@humanrights.or.tz