Uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Kuhusu Shauri Namba 18130/2026 (TLS, LHRC na Dkt. Slaa Dhidi ya Patrobas Katambi ).

Uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Kuhusu Shauri Namba 18130/2026 (TLS, LHRC na Dkt. Slaa Dhidi ya Patrobas Katambi ).

Posted 12 hours ago

Mnamo tarehe 4 Novemba 2026,

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Tabora, ilitoa uamuzi kuhusu pingamizi za awali zilizowasilishwa na pande pande zote katika shauri lililofunguliwa na Tanganyika Law Society (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) pamoja na Dkt. W. P. Slaa dhidi ya Patrobas Katambi na wengine kesi namba 18130 of 2026. Maamuzi hayo yametolewa na jopo la majaji watatu ambao ni; Mheshimwa Jaji Alfan, Mheshimiwa Jaji Mgeta na Mheshimiwa Jaji Mpaze,

Katika mapingamizi matano (5) yaliyowasilishwa na upande wa Serikali, Mahakama ilikubali pingamizi moja tu lililohusu kukosekana kwa msingi wa kisheria wa kuwashitaki wadhamini wa CHADEMA na ACT Wazalendo katika shauri hili. Kutokana na uamuzi huo, CHADEMA na ACT Wazalendo wameondolewa rasmi katika shauri hilo.

Kwa upande mwingine, Mahakama ilikubali pingamizi zote mbili zilizowasilishwa na upande wa waleta maombi kuhusu uhalali wa majibu na hati ya kiapo ya kupinga (Reply and Counter-Affidavit) zilizowasilishwa kwa niaba ya Patrobas Katambi. Mahakama ilibaini kuwa nyaraka hizo hazikuwa na uhalali wa kisheria. Hivyo, ikaamuru nyaraka hizo ziondolewe katika kumbukumbu za shauri.

Baada ya uamuzi huo, Mahakama imeelekeza kuwa shauri liendelee kwa njia ya maandishi kwa kuzingatia ratiba ifuatayo;

1. Mawasilisho ya awali yawasilishwe kabla au ifikapo tarehe 11 Novemba 2026, majibu yawasilishwe kabla au ifikapo tarehe 18 Novemba 2026, 2. Ufafanuzi wa hoja zozote zinazohitaji kujadiliwa ufanyike mahakamani tarehe 10 Desemba 2026, saa 4:00 asubuhi.

Mahakama imekubali pingamizi moja la Serikali na kuondoa CHADEMA na ACT Wazalendo kwenye shauri, lakini pia imekubali pingamizi zote mbili za waleta maombi na kufuta majibu pamoja na hati ya kiapo vilivyowasilishwa kwa niaba ya Patrobas Katambi.

Upande wa waleta maombi unawakilishwa na Jopo la Mawakili kutoka Kituo cha Sheria na Haki Binadamu na Chama cha Mawakili wa Tanganyika likiongozwa na Wakili Msomi Mwandamizi Mpale Kaba Mpoki, Wakili Jebra Kambole na Wakili Edson Kilatu.